Friday, 19 September 2014

N/WAZIRI FEDHA MWIGULU NCHEMBA "JINO KWA JINO KWA WANAOHUJUMU FEDHA ZA UMMA KUPITIA MISHAHARA HEWA"

Waliosababishia Serikali hasara ya bn 40/- kukiona

Naibu Waziri wa Fedha, Mungulu Nchemba
Wizara ya Fedha imeziagiza taasisi zilizokabidhiwa jukumu la kuchunguza wakuu wa mashirika na taasisi za umma waliojihusisha katika kughushi malipo hewa ya wafanyakazi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 40 kila mwezi wafichuliwe.
 
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mungulu Nchemba, akisema wakuu hao pamoja na waajiri wametumia mwanya wa wafanyakazi wao katika  ubadhirifu wa fedha kwa maslahi yao binafsi.
 
Kadhalika, wizara inawataka maafisa utumishi na waajiri kuhakiki upya taarifa wanazoweka katika mfumo ni sahihi ili watumishi wao wawekewe malipo yao katika akaunti kwa wakati mwafaka.
 
“Zoezi hili ni endelevu, hivyo tumebaini tatizo na tunatafuta njia ya kulimaliza na  hii tuliyowaagiza waajiri itakuwa njia ya kutokea, hivyo tutalinganisha taarifa zao na muda wa watumishi wao tuone tatizo lilikuwa wapi,” alisema.
 
Pia, alisema hakuna sababu ya wizara kuendelea kulipa malipo hewa wakati kuna kundi la wafanyakazi katika taasisi na mashirika hayo, ambao kazi yao ni kuhakiki mafaili na wanalipwa mishahara mikubwa huku wale wanaojituma wakiendelea kujaziwa  mishahara hewa.
 
Aliwaagiza waajiri na maafisa hao kufikisha orodha ya majina ya watumishi wakiambatanisha na taarifa sahihi ya mishahara tarehe za mwanzo za kila mwezi zifanyiwe kazi mapema ili kuwepo na uwajibikaji katika sehemu za kazi.
 
Alisema fedha za miradi katika taasisi hizo zitatolewa kulingana na mchanganuo wa malipo yao, “Hatuwezi kuendelea kutoa  malipo hewa kinyemela  tena, hivyo wataalamu wetu watashirikiana na wakuu hao wa maradi kuangalia kama unakidhi kutekelezewa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment