Monday 9 February 2015

KUELEKEA 2015,MWIGULU NCHEMBA ANG'ARA KUWANIA NAFASI YA JUU YA UONGOZI WA NCHI,TEDRO WATOA RIPOTI YAO

Wasaka urais vijana: Utafiti wamng'arisha Mwigulu


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Harakati za Uchaguzi Mkuu zimeendelea kushika kasi, baada ya utafiti uliotolewa jana kumtaja Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kuongoza kundi la wanasiasa vijana wanaokubalika na Watanzania katika kugombea nafasi ya urais.
Akizungumza jijini Dar es salaam jana
wakati akizindua ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Elimu (Tedro), Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Jacob Kiteli, alisema Nchemba aliongoza kati ya wanasiasa vijana saba waliotajwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani.
Alisema utafiti huo ulifanyika katika wilaya 18 na vijiji 54, ulikuwa na lengo la kutathimini ushiriki wa vijana katika siasa katika kugombea na kutekeleza wajibu wao kwenye madaraka kwa maendeleo ya jamii.
Alisema katika kipengele cha mtu gani anaweza kupita katika uchaguzi endapo CCM itampendekeza, Nchemba alipata asilimia 38 na kufuatiwa na January Makamba aliyepata alama ya asilimia 24.
Wengine waliotajwa na alama zao kwenye mabano ni William Ngeleja (11), Lazaro Nyalandu (10), Dk. Hamisi Kigwangallah (7), Deo Felikunjombe (5) na Esther Bulaya (2).
Utafiti huo pia umebaini kuwa mgombea kijana ambaye angeshinda kwenye kinyang’anyiro hicho bila kujali itikadi za vyama, Nchemba ameongoza kwa asilimia 27, akifuatiwa na Zitto Kabwe (Chadema) kwa asilimia 19.
Wengine na asilimia zao kwenye mabano ni Makamba (14), James Mbatia (10), Tundu Lissu (14), Nchimbi (8) na Nyalandu (7).
Kwa upande wa upinzani, vijana wanaoonekana kuwa na ushawishi mkubwa ni Zitto (19), Mbatia (11), Lissu (5) na Halima Mdee (4).
Akizungumzia kuhusu chama chenye nafasi kubwa ya kushinda iwapo uchaguzi ungefanyika leo, Kiteli alisema utafiti umebaini kuwa CCM bado ina nafasi kubwa ikiongoza kwa asilimia 53.4.
Katika kundi hilo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinafuatia kwa asilimia 27. 3, kikifuatiwa na Cuf (7.3) na NCCR-Mageuzi (4.4).
Kiteli alisema Watanzania wengi wana amini vijana wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na kisiasa.
“Asilimia 82 ya waliohojiwa walikubali kumpigia kura mgombea urais kijana, 11 walikataa na saba walisema hawajui,” alisema. 
Alisema utafiti huo unaonyesha katika chaguzi vijana wengi waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali, baadhi yao walishinda na wengine kushindwa.
“Sababu ya vijana kushindwa katika uchaguzi inatokana na kukosa fedha za kuendesha kampeni, kutojipanga vyema kukabiliana na wapinzani wao pamoja na kupewa rushwa ili wajitoe,” alisema Kiteli.
Hata hivyo, Kiteli alifafanua kwamba utafiti huo haukuegemea vyama vya kisiasa wala makundi ya kijamii, badala yake iliegemea kujua mahitaji ya wananchi juu ya viongozi wanaowahitaji. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment