Saturday, 2 November 2013

JK,SERIKALI KUENDESHWA KWA UWAZI ZAIDI

JK : SERIKALI KUENDESHWA KWA UWAZI ZAIDI

MABADILIKO yanatarajiwa kufanyika nchini kuhusu suala zima la uwazi katika uendeshaji wa Serikali huku ikitarajiwa mambo mbalimbali ikiwemo mishahara kutokuwa siri. Rais Jakaya Kikwete alisema juzi mjini London – Uingereza, kwamba mabadiliko hayo si kwa sekta ya umma pekee, bali pia binafsi ambako kila anayejihusisha na umma hususani mashirika yasiyo ya serikali (NGO), anapaswa kuweka wazi vyanzo vya mapato, kiasi cha fedha alichopewa na matumizi yake.

Katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari, Rais alisema ingawa ipo changamoto ya kubadili mazoea yaliyopo ya kila kitu serikalini kuendesha kwa usiri, anaamini mabadiliko yatakuwapo ndani ya miaka miwili ijayo na hadi anatoka madarakani 2015, kila kitu katika uendeshaji Serikali kitakuwa wazi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Uendeshaji Serikali kwa Uwazi (OGP) ulioanzishwa na Rais wa Marekani, Barack Obama na Tanzania kujiunga nao mwaka 2011. Rais Kikwete na ujumbe wake, alikuwa hapa kuhudhuria mkutano wa mwaka wa OGP ulioanza Oktoba 31 na kumalizika jana.

Mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki 1,000 kutoka nchi 60 wanachama na Rais Kikwete alipata nafasi ya kuueleza mkutano huo, namna Tanzania ilivyoanza utekelezaji wa masharti ya mpango huo.

“Mshahara hauwezi kuwa siri. Si ipo kwenye bajeti za Serikali?” Alijibu Rais Kikwete alipoulizwa kama suala la mishahara litaendelea kuwa siri katika utekelezaji wa mpango huo. Kikwete alisema:

“Changamoto iliyopo ni kwamba mpango huu unabadili mazoea yetu ya kufanya kazi. Sisi katika kila serikali kila kitu ni siri. Sasa OGP inataka mambo haya yawe wazi; ifike hatua mtu aone kutoa habari ni wajibu.” Alisema alifurahi Rais Obama alipomwambia Tanzania ina sifa ya kujiunga na umoja huo.

Alisema aliona ni jambo jema serikali iliyo chini ya wananchi kujiendesha kwa uwazi tofauti na mfumo uliotawala ambao ni wa usiri. Kibano halmashauri Miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mpango alizotaja Rais Kikwete, ni pamoja na uwazi kwenye bajeti ya serikali.

No comments:

Post a Comment